Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limemkabidhi cheti cha shukrani Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya (Mbeya DC), Bi. Erica Yegella, kwa kutambua mchango wake katika ujenzi wa Kituo cha Polisi Igoma.
Akikabidhi cheti hicho leo, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Christopher Msonsa, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RPC), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, amesema kuwa cheti hicho kimetolewa kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango muhimu wa Halmashauri katika kuimarisha ulinzi na usalama, na hivyo kuchangia kudumisha amani na utulivu katika jamii.
Cheti hicho, kilichotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya na kusainiwa na RPC, kinaeleza kutambua na kuthamini juhudi za Mkurugenzi wa Mbeya DC katika kuimarisha usalama, mshikamano wa jamii, upatikanaji wa huduma bora, pamoja na maendeleo ya wananchi.
Aidha, Jeshi la Polisi limemshukuru Bi. Yegella kwa ushirikiano wake wa hali na mali wakati wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Igoma. Mbali na mchango wa kifedha na kiufundi, Halmashauri pia ilitoa samani kwa ajili ya kituo hicho, hatua iliyosaidia kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa askari na watumishi wa kituo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mbeya DC, Bi. Erica Yegella, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kutambua mchango wa Halmashauri katika kuimarisha ulinzi na usalama. Amesema kuwa ulinzi ni msingi wa maendeleo, kwani unahakikisha usalama wa raia na mali zao; hivyo, Halmashauri haikusita kushiriki kikamilifu katika ujenzi na uwezeshaji wa Kituo cha Polisi Igoma.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.