Wakulima wa Kata ya Isuto, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya (Mbeya DC), leo wamepatiwa bure jumla ya miche ya kahawa bora na ya kisasa 71,000, kupitia ruzuku ya asilimia 100 iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Sambamba na ugawaji wa miche hiyo, wakulima hao wamepatiwa pia elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa ajili ya uzalishaji wa mazao mbalimbali, ikiwemo kahawa, ambayo ni miongoni mwa mazao muhimu ya biashara katika halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi miche hiyo kwa wakulima wa vyama viwili vya ushirika; Chama cha Ushirika Shinzingo (Shinzingo AMCOS) na Chama cha Ushirika Umalila (Umalila AMCOS) kutoka vijiji vya Shizingo na Umalila mtawalia, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Mbeya, Cuthbert Mwinuka, amesema Serikali imeweka mkakati wa kutoa miche ya kahawa yenye ruzuku ili kuwawezesha wananchi kupata mbegu bora na za kisasa zitakazoongeza uzalishaji.

“Miche hii tuliyotoa leo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao mengi katika eneo dogo la ardhi, tofauti na mbegu za zamani. Mche mmoja unaweza kutoa mavuno ya wastani wa kilo moja (1) hadi kilo tano (5) za kahawa. Aidha, upandaji wake hauhitaji nafasi kubwa, hivyo katika hekari moja (1) mkulima anaweza kupanda hadi miche 1,000. Hii humwezesha mkulima kuvuna mazao mengi zaidi endapo atazingatia kanuni bora za kilimo,” amesema Mwinuka.
Kwa upande wake, Mtaalam wa Kilimo kutoka Kampuni ya Minjingu Mines and Fertiliser Limited, Juma Kayeke, amesema kampuni hiyo imeamua kushirikiana na halmashauri kuhakikisha wakulima wanapatiwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakati muafaka, ili kusaidia ukuaji mzuri wa miche hiyo na kufanikisha uzalishaji uliokusudiwa.
“Sisi kama Minjingu Mines and Fertilizer Limited, tumekuwa tukizalisha mbolea kwa ajili ya mazao mbalimbali, ikiwemo kahawa. Leo tumetoa mbolea kwa vyama viwili vya ushirika katika kata hii kwa ajili ya mashamba ya mfano, ambayo yatasaidia wakulima kujifunza na kufanya maamuzi sahihi, ikiwemo matumizi ya mbolea zinazozalishwa na kampuni yetu,” amesema Kayeke.
Diwani wa Kata ya Isuto, Veronica Mzumbwe, ameishukuru Serikali kupitia halmashauri kwa jitihada kubwa ya kugawa miche ya kahawa kwa wananchi, akisema hatua hiyo itaongeza uzalishaji wa zao hilo kutokana na upatikanaji wa mbegu bora bure, kupitia ruzuku iliyowekezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Naye Meneja wa Chama cha Ushirika Shizingo kutoka Kijiji cha Shizingo, Ntuta Mwozya, ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha wakulima kupata miche ya kahawa bure pamoja na elimu ya matumizi ya mbolea, hatua itakayosaidia uzalishaji wa kahawa bora na yenye ubora wa juu zaidi.
Kwa upande mwingine, Mjumbe na Mwakilishi wa Chama cha Ushirika cha Umalila, Philemon Mwanijembe, amepongeza jitihada za Serikali katika kutoa ruzuku hiyo, akisema imeonesha dhahiri kujali maslahi ya wananchi wengi wanaotegemea kilimo kama chanzo kikuu cha maisha yao.

Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.