Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango imehitimisha leo ziara yake ya siku tatu kwa kukagua vikundi vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, pamoja na kufanya ukaguzi wa Kituo cha Afya Mbalizi.
Katika ziara hiyo, Kamati ilitembelea vikundi mbalimbali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyopata mikopo hiyo, kwa lengo la kujiridhisha na matumizi sahihi ya fedha, utekelezaji wa miradi pamoja na uendelevu wake. Kamati ilipata fursa ya kusikiliza taarifa za wanufaika na kujionea maendeleo yaliyopatikana kutokana na mikopo hiyo.
Aidha, Kamati ilikagua Kituo cha Afya Mbalizi ambapo ilipitia hali ya utoaji wa huduma za afya, miundombinu, upatikanaji wa vifaa tiba na rasilimali watu, sambamba na kusikiliza changamoto zinazokikabili kituo hicho.
Akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Aidda C. Haule, ameipongeza menejimenti ya Halmashauri kwa usimamizi na ufatiliaji mzuri wa miradi ya mikopo ya asilimia 10 pamoja na juhudi zinazoendelea za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
“Menejimenti imefanya kazi nzuri katika kuhakikisha mikopo inawafikia walengwa na inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Hii imechangia kuinua kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” alisema Mhe. Haule.

Kamati imeendelea kutoa maelekezo na ushauri ili kuboresha zaidi usimamizi wa miradi hiyo, ikiwemo kuimarisha ufuatiliaji wa mara kwa mara na kutoa elimu ya usimamizi wa fedha kwa wanufaika, ili kuhakikisha mikopo inaleta tija endelevu kwa jamii.
Mbaliz Road
Postal Address: 599
Telephone: 025-2502260
Mobile: 0762210758
Email: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.