Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya (Mbeya DC) imesajili jumla ya wananchi 483 katika Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, kutoka kundi la wananchi wasio na uwezo wakiwemo wazee, watoto na wajawazito. Wananchi hao wanagharamiwa moja kwa moja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Afisa Uanachama Mwandamizi kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa niaba ya Meneja wa NHIF Mkoa wa Mbeya, Calistus Mpangala, wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mbeya DC kilichoketi kujadili na kupitisha Rasimu ya Mapendekezo ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Akizungumza katika kikao hicho, Mpangala amesema NHIF inaendelea na zoezi la usajili wa wananchi kutoka kaya masikini, ikiwemo zile zinazotambuliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Amesema zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maono na ahadi ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2025, ya kutekeleza mpango huo ndani ya siku 100 endapo angechaguliwa.
“Naomba niwasihi Waheshimiwa Madiwani kuendelea kuhamasisha kaya zote zilizo katika mpango wa TASAF kwenye maeneo yao zijitokeze kwa ajili ya usajili, ili tuweze kutekeleza kikamilifu azma hii kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais,” amesisitiza Afisa Uanachama Mwandamizi wa NHIF.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, Mbeya DC ina jumla ya wananchi 3,944 wanaotoka katika kaya masikini. Hadi sasa, wananchi 483 tayari wameshasajiliwa katika Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, huku zoezi likiendelea katika kata za Igonza, Ulenje na Ilungu, kwa lengo la kuhakikisha agizo la Mheshimiwa Rais linatekelezwa kwa ufanisi.
Aidha, Mpangala amebainisha kuwa kitaifa, Tanzania inakadiriwa kuwa na zaidi ya kaya masikini milioni 3.7. Hata hivyo, kaya zinazotambulika rasmi hazizidi 900,000. Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, Serikali imefanikiwa kugharamia usajili wa kaya takribani 278,000.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.