Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Solomoni Itunda Akutana na Machifu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya
Mbeya, Agosti 28, 2025 – Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomoni Itunda, amekutana na kufanya mazungumzo na machifu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, waliokuwa wakiongozwa na Katibu wa Machifu, Chifu Akida Wabu Mtondo wa Pili kutoka mkoa wa Ruvuma.
Katika kikao hicho, Mhe. Itunda aliwashukuru machifu hao kwa kuitikia wito wa kukutana naye na kuwataka kushiriki katika mapokezi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yatakayofanyika hivi karibuni katika eneo la Mbalizi Mkoani Mbeya.
Aidha, DC Itunda aliwasihi machifu kuendelea kusimamia maadili na utamaduni wa Kitanzania katika jamii, na kutokuvumilia wala kuwafumbia macho watu wanaotoa kauli za kejeli dhidi ya Serikali ya awamu ya sita.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Itunda pia aliwaalika machifu kushiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mwezi Oktoba, ambapo mwenge huo utazimwa kitaifa katika Jiji la Mbeya, na Mhe Rais.
Kwa upande wake, Chifu Akida Wabu Mtondo alitoa shukrani kwa Mkuu wa Wilaya kwa kuitisha kikao hicho muhimu na kuahidi kuwa machifu wapo tayari kushirikiana bega kwa bega na serikali katika masuala yote ya kijamii na maendeleo ya taifa.
Kikao hicho kimelenga kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na viongozi wa kimila katika kutunza mila, amani na maadili ya jamii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.