Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Beno Malisa, amewataka wananchi mkoani humo kuachana na nishati chafu na kuendeleza matumizi ya nishati safi kwa madai kuwa Serikali imeandaa mazingira rafiki ili kuboresha mazingira na kurejesha uoto wa asili.
Agizo hilo la mkuu wa mkoa wa Mbeya limetolewa kwa niaba yake na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Bi. Erica Yegella wakati akizungumza kwenye kongamano la matumizi ya nishati safi lililoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali TAWEN.
Akimwakilisha mkuu huyo wa mkoa, bi. Yegella amesema matumizi ya nishati safi ni msingi wa maendeleo kwani nishati chafu hasa kuni na mkaa vimekuwa vikiathiri mazingira kutokana na ukataji miti hovyo na kuathiri pia maisha ya wananchi jambo ambalo limetazamwa na Serikali ya awamu ya sita na kulivalia njuga ili kuachana na matumizi ya nishati chafu.
Amesema ziko fursa mbalimbali kutoka Serikalini na sekta binafsi ikiwemo upatikanaji wa majiko ya umeme, gesi kutoka kwa wawekezaji mbalimbali na mkaa utokanao na makaa ya mawe.
Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la Tanzania Women Empowerment Network (TAWEN) Taifa Frolence Masunga, amesema lengo la shirika hilo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu ambapo wamefika katika Halmashauri ya Mbeya na kushirikiana na Halmashauri na wadau wengine mbalimbali ili kufikisha elimu hiyo kwa wanajamii.
Amesema kwa mwaka zaidi ya watu elfu thelathini hufariki Dunia kutokana na kuendekeza matumizi ya nishati chafu hivyo shirika hilo linazunguka kote Tanzania ili kuelimisha wananchi kujiandaa na kuanza kuhama kwenye matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa ili kutunza mazingira.
Baadhi ya wananchi walioshiriki hafla hiyo wameiomba Serikali ya Tanzania kusaidia kupunguza bei ya vitendea kazi vitakavyowasaidia kwenye matumizi ya nishati safi kutokana na wengi wa wa-Tanzania kuwa na hali ngumu ya kiuchumi hivyo kushindwa kumudu gharama za kununua vifaa kama majiko ya umeme na gesi.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.