Katika kuadhimisha siku ya mazingira Duniani, Halmashauri ya wilaya ya Mbeya imeungana na wananchi wengine kufanya usafi wa mazingira na kuhimiza utunzaji bora wa mazingira kwa ustawi wa Tanzania ya sasa na ijayo.
Shughuli ya usafi katika mji wa Mbalizi hasa kuzunguka eneo la mto Mbalizi imeongozwa na kaimu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mbeya John Maholani.
Akizungumza na wananchi wa mji wa Mbalizi na Mbeya kwa ujumla, Maholani amewataka wananchi kujenga tabia ya usafi kuwa desturi badala ya kusubiri kuhimizwa na kuhakikisha idara ya mazingira na watendaji kata wanasimamia zoezi hilo.
Afisa mazingira kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mbeya John Rulala amesema wataendelea kufanya doria na kuchukua hatua kwa wanaokiuka kanuni na sheria walizojiwekea huku akisisitiza wananchi kuzingatia elimu ya utunzaji mazingira badala ya kusubiri kutozwa faini zisizo na msingi.
Kwa upande wake mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi Daudi Mbembela amewataka wananchi wa Mbeya vijijini hasa katika mamlaka hiyo ya mji mdogo kushirikiana na viongozi wao kutunza mazingira na kutotupa taka hovyo ili kuepukana na magonjwa mbalimbali hasa ya mripuko.
Viongozi mbalimbali wa kata vitongoji wamewataka wananchi kila mmoja kuhakikisha anakuwa na eneo la kukusanyia taka taka na kukusanya kwenye gari la kuzoa taka kulingana na ratiba walizojiwekea ili kuhifadhi mazingira.
Nao wananchi waliozungumzia maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani wamesema uchafu unachagizwa na baadhi ya wananchi ambao wanaenda kutupa taka hovyo hasa maeneo ya wazi na kwenye kingo za mto bila kujali usalama wa afya zao na kutaka suala la usafi liwe endelevu badala ya kusubiri maadhimisho ya mazingira au siku za usafi.
Siku ya mazingira Duniani huadhimishwa Juni 04 kila mwaka kote ulimwenguni ili kutafakari kwa pamoja juu ya uhifadhi bora wa mazingira, changamoto na mafanikio katika suala la mazingira pamoja na hatua mahususi za kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa ipasavyo ili kutunza uoto wa asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kile cha Tanzania ijayo.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.