Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inaongozwa na Baraza la Madiwani ambacho ndicho chombo kikuu cha maamuzi. Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya za Mwaka 2013 kanuni ya 40 (1) Halmashauri kupitia mkutano wa mwaka itateua wajumbe wa kamati mbalimbali za kudumu, ikiwema kamati ya Fedha, Ungozi na Mipango (FUM).
WAJUMBE WA KAMATI YA FEDHA, UONGOZI NA UTAWALA
Kama ilivyoelezwa hapo juu kuwa kupitia Mkutano wa Mwaka Baraza la Madiwani linajukumu kubwa ya kufanya uteuzi wa wajumbe wa kamati mbalimbali za kudumu za Halmashauri. Lakini tofauti na kamati nyingine wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (FUM) wanateuliwa kulingana na vyeo vyao kama ilivyobainishwa kwenye kanuni ya 40 (2) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya za Mwaka 2013.
Kanuni ya 40 (2) inaeleza
“Kila Mjumbe wa Halmashauri atakuwa Mjumbe wa angalau Kamati moja ya Kudumu. Kamati ya Fedha na Utawala itakuwa na Wajumbe wafuatao-
Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye atakuwa Mwenyekiti.
Makamu Mwenyekiti
Mbunge au Wabunge wa Majimbo wanaowakilisha Majimbo katika eneo la Halmashauri
Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Halmashauri
Wajumbe wengine wasiozidi wawili(2) watakaopendekezwa na Mwenyekiti na kupigiwa kura na Baraza la Halmashauri mmoja kati yao awe Mwanaume".
Kanuni ya 40 (5) inaeleza
“Bila kuathiri masharti ya Kanuni Ndogo ya (2)(3) na (4) ya Kanuni hii, Halmashauri yenye idadi ya Madiwani wanaozidi thelathini na tano(35) na zaidi Wajumbe wa Kamati ya Fedha watakuwa kama ilivyoonyeshwa kwenye Kanuni ya 40(2) pamoja na wajumbe wengine wanne(4) watakaotokana na orodha itakayopendekezwa na Mwenyekiti na kupigiwa kura na Baraza la Halmashauri wawili kati yao wawe wanawake”
Ifuatayo ni orodha ya wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kwa Mwaka 2017/2018
Orodha ya wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango.pdf
MAJUKUMU YA KAMATI YA FEDHA, UONGOZI NA MIPANGO.
Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango inatekeleza majuku yake kisheria kama yalivyobainishwa kwenye Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya za Mwaka 2013. Majukumu hayo ni kama ifuatavyo:
Kuweka mikakati na kupendekeza uongezaji wa mapato
kuwasilisha mapendekezo ya Bajeti na mpango wa Maendeleo kwenye Halmashauri ili kuidhinishwa na Halmashauri.
kusimamia utunzaji wa hesabu za fedha ikiwa ni pamoja na uhakiki wa mali za Halmashauri, ukusanyaji wa mapato, kufuta madeni, na kuomba vibali Maalum kwa matumizi yanayohitaji kibali cha Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa.
kufikiria na, pale inapowezekana, kupendekeza kwenye Halmashauri masuala yanayohusu Sheria Ndogo na utendaji katika ngazi za chini za Halmashauri.
kupokea na kuzingatia mapendekezo ya kubadili matumizi ya mafungu ya fedha (re-allocation) yaliyopo katika makisio yaliyoidhinishwa na kuyapeleka kwa Halmashauri.
kuratibu mapendekezo kutoka kwenye Kamati zingine kuhusu matumizi ya kawaida na miradi na kuyawasilisha kwenye Halmashauri.
kufikiria na kupendekeza kwenye Halmashauri mikopo yote ya Halmashauri.
kutoa mapendekezo ya vitega uchumi kwa madhumuni ya kuongeza mapato kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290.
kupokea na kujadili taarifa za wakaguzi wa fedha na mali ya Halmashauri na kupendekeza hatua za kuchukuliwa kutokana na maelekezo na maoni ya wakaguzi kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa, Sura ya 290.
Kusimamia na kudhibiti matumizi ya fedha za Halmashauri, kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Waziri na taratibu nyingine zitakazowekwa na Halmashauri;
Kupitia marekebisho yote yaliyopendekezwa hususan kuhusu taratibu za fedha, ikiwa ni pamoja na mapitio ya mara kwa mara yanayohusu thamani ya fedha ambapo Kanuni mbalimbali za manunuzi ya mali na vifaa hutumika;
Kufikiria na kupendekeza mabadiliko ya viwango vya kodi, ada na ushuru mbalimbali, vinavyotolewa na Halmashauri;
Kufikiria mapendekezo ya Bajeti na Mipango ya Maendeleo ya kila Kamati ya Kudumu na kuiwasilisha kwenye Halmashauri ili kupata idhini;
Kushughulikia tofauti ya mapato na matumizi katika bajeti yote na kupendekeza hatua stahiki ya kuchukua kuondoa mapungufu katika mapato au ziada matumizi;
Kufikiria mapendekezo yote yanayohusu matumizi makubwa ya fedha kabla hayajawasilishwa kwenye Halmashauri ili kupata idhini;
Kupokea mahesabu ya mwaka ya Halmashauri na kuhakikisha taarifa ya mahesabu ya mwaka inawasilishwa kwa wakati kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali;
Kupitia na kuidhinisha mpango wa manunuzi wa Halmashauri kwa kuzingatia mpango wa Bajeti uliopitishwa na Halmashauri;
Kupitia taarifa ya kila robo mwaka kuhusu Manunuzi iliyowasilishwa na Afisa Masuuli;
Kusimamia utekelezaji wa mikataba ya Halmashauri kwa kukagua miradi inayotekelezwa na vifaa vilivyopokelewa;
Kumwelekeza Mkurugenzi kufanya manunuzi au ukaguzi wa huduma au vifaa vilivyonunuliwa ili kupata thamani halisi, itafanyika hivyo endapo itadhihirika kwamba, maelezo yaliyotolewa kuhusu manunuzi ya vifaa au huduma hayaridhishi;
Kuidhinisha majina ya wajumbe wa Bodi ya zabuni na wa Bodi zingine kwa mujibu wa Sheria husika;
Kushughulikia orodha ya wadaiwa wote itakayokayowasilishwa kwenye Kamati na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua;
Kupendekeza njia na taratibu za kuondosha vifaa chakavu. Uondoshaji wa vifaa unaweza kufanyika kwa njia ya kuuza au kuviharibu;
Kujadili na kupitia taarifa za fedha za kila mwezi na kila robo mwaka
Kupendekeza kwa Halmashauri hatua za kuchukua kuhusu kufuta madeni ya Halmashauri;
Kushughulikia Sera kuhusu kukopa na uwekezaji,
Kujadili na kupendekeza mabadiliko ya viwango vya kodi, ada na ushuru mbalimbali vinavyotozwa na Halmashauri,
Kubuni na kupendekeza mpango wa kuanzisha na kuendeleza uhusiano na Halmashauri nyingine.
Kurekebisha na kusimamia makusanyo na matumizi ya mapato ya vijiji na miji midogo kwa mujibu wa Sheria, Sura ya 287.
kuteua wakaguzi wa fedha/mali za Serikali za Vijiji kwa mujibu wa Sheria, Sura ya 290.
Kujadili na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa kuhusu mambo yote ya yanayohusu masuala ya ajira na kinidhamu ya wafanyakazi na watumishi.
Kujadili na kutoa mapendekezo kuhusu masuala yanayohusu nyumba za Halmashauri.
Kupokea na kutoa uamuzi juu ya mapendekezo ya watumishi wanaokwenda masomoni.
Kujadili na kupendekeza masuala yote yanayohusu maslahi ya jumla ya watumishi, ikiwa ni pamoja na mikopo, nyumba, usafiri, matibabu, rambirambi na motisha nyinginezo.
Kupitisha mapendekezo ya kuthibitisha watumishi kazini baada ya kumaliza kipindi cha majaribio kulingana na miundo husika ya utumishi.
kupendekeza Sheria Ndogo zinazohusu Kamati hii
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.