MAADHIMISHO SIKU YA WAZEE MBEYA DC
Na Fatina Msangi
Halmashauri ya wilaya ya Mbeya imeadhimisha siku ya wazee duniani kwa kuwakutanisha wazee kutoka maeneo mbalimbali wilayani humo ili kutafakari mchango wao katika Taifa na changamoto zinazowakabili.
Katibu wa baraza la wazee kata ya Inyala Jesko Linga akiwasilisha taarifa ya wazee hao ameishukuru Serikali kwa uimarishaji miundombinu mbalimbali ya wazee na kuomba kutatuliwa kwa baadhi ya kero zinazowakabili.
Baadhi ya kero hizo ni pamoja na uboreshaji madirisha ya wazee kwa kuhakikisha dawa zinapatikana hasa vijijini.
Akijibia suala hilo mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya Mhe. Mwalingo Kisemba amesema dawa zinapatikana kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali mbalimbali kulingana na ukubwa wa eneo husika la utolewaji huduma.
"Hapa kwenye afya naomba mnisikilize Serikali inajitahidi kuleta dawa sema tofauti ni viwango, ukienda zahanati huwezipata kwenye kituo cha afya na ukienda kituo cha afya kuna dawa utazikosa hadi wilaya na baadaye hospitali ya rufaa ya mkoa na sisi tuna bahati hospitali ya wilaya iko hapahapa Inyala hadi kifaa kinaitwa Utra-sound kipo hapa kwa ajili ya kupima vitu vya ndani ya mwili bila kuingia ndani kwa hiyo mnaona namna gani Serikali imeboresha huduma za afya", amesema Mwalingo Kisemba.
Mwenyekiti wa Baraza la wazee wilaya ya Mbeya Filmon Nswila, ameomba agenda na maombi yao yatiliwe maanani na Serikali ili kufanyiwa maboresho hasa kwa kuthamini mchango wa wazee katika Taifa ambapo amesema mapendekezo yao yote wameyawasilisha kupitia maadhimisho ya kitaifa yaliyofanyika mkoani Tabora.
Kuhusu mapendekezo ya kuboreshwa na kuundwa kwa sheria za wazee, mgeni rasmi huyo ameeleza kupokea mapendekezo ya wazee wa wilaya ya Mbeya na kuahidi kumfikishia mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza ili kuona namna ya kufikisha juu mapendekezo yao ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sheria kadhaa juu ya kundi hilo muhimu katika jamii.
Oktoba mosi ya kila mwaka, Dunia huadhimisha siku ya Wazee, siku ambayo ilianzishwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 14 Desemba 1990.
Maadhimisho haya ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Vienna wa Mwaka 1982 kwa ajili ya wazee kote Duniani, “The Vienna International Plan of Action on Ageing” ulioboreshwa tena na mkakati wa Madrid, Hispania wa Mwaka 2002 ili kupambana na changamoto za wazee katika Karne ya 21 na kuendelea na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa ajili ya wote.
Kaulimbiu ya mwaka huu 2024 ni "TUIMARISHE HUDUMA KWA WAZEE WAZEEKE KWA HESHIMA".
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.