Mapema leo tarehe 05 Januari, 2024 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Afisa Tawala Mkoa wa Mbeya ndugu Rodrick Mpogolo pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya wamesaini Mkataba wa Upimaji wa Utendaji Kazi kupitia mfumo wa Upimaji Watumishi PEPMIS ambao ni mbadala wa Mfumo wa OPRAS uliokuwa ukitumika kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2021.
Wakurugenzi wamesaini Mkataba huo ikiwa ni ishara ya kuanza kutekeleza Mfumo wa Upimaji utendaji kazi katika Utumishi wa Umma Kidijitali na kumhakikishia Afisa Tawala utendaji kazi mzuri na ulotukuka na kuwa watawasimamia watumishi walio chini yao kuweza kutekeleza majukumu yao ya kila siku na kutoa taarifa ya utendaji kazi wao kupitia mfumo PEPMIS.
Mfumo PEPMIS ni Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma (Public Employees Performance Management Information System – PEPMIS) unaohusisha hatua tano zinazotegemeana ambazo ni Kuandaa Mpango wa Utendaji Kazi wa Taasisi wa Mwaka; Kutekeleza na Kufuatilia Mpango wa Utendaji Kazi wa Taasisi wa Mwaka; Kuhuisha Mpango wa Utendaji Kazi wa Mwaka; Kufanya Tathmini ya Utendaji Kazi wa Watumishi na Kukata Rufaa ya Matokeo ya Tathmini ya Utendaji Kazi wa Mtumishi wa Umma. Inategemewa kwamba, utekelezaji wa mfumo huu utarahisha utendaji kazi wa watumishi wa Umma na kuongeza uwajibikaji wa kila mtumishi kwa Umma na kwa Serikali.
Mfumo huu utatumika kwa watumishi wote wa umma Nchini, ukianzia na Mkuu wa Taasisi, Wakuu wa Idara na Vitengo, Wakuu wa Sehemu na kufatiwa na watendaji wote walio chini yao, ambapo mfumo utamtambua kazi zilizopangwa na kutekelezwa na kila mtumishi na kuzipima na hatimaye mtumishi kupata alama kutokana na utekelezaji wa Kazi alizopanga na alizofanya kwa mwaka husika.
Aidha, Katibu Tawala Mkoa amewataka Watumishi wote kuhakikisha kwamba wanautumia Mfumo huu kwa kuwa Utaleta mapinduzi ya Utendaji wa Serikali kwa kuongeza ufanisi na kuboresha huduma kwa Wananchi wanaotumia huduma zitolewazo na Watendaji Serikalini. Katibu Tawala Mkoa amesifu jitihada zinazofanywa na Serikali zikisimamiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia S. Hassan na kuwapongeza watumishi walioupokea na kutimiza wajibu wao kwa kuandaa mipango ya Utendaji kazi wa Mwaka.
Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya amewataka Watumishi wote wa Mkoa wa Mbeya kuutumia Mfumo huu na kutekeleza kauti mbiu yake inayosema. ”PEPMIS - TUJENGE UTUMISHI WA UMMA WA KIDIJITALI”
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.