Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya Mbeya ndug Stephen E. Katemba ametembelea kituo cha afya Ilungu na kuwatangazia kuwa kituo hicho kitafunguliwa rasmi tarehe 15/11/2023. Ni kilio cha muda mrefu cha wanakijiji hao kuiomba serikali kukifungua kituo hicho cha afya.
Katemba ameyasema hayo kwenye mkutano na wanakijiji walio kuwa wamekusanyika kwenye zahanati hiyo. “kuanzia wiki ijayo mhandisi atakuwepo hapa kuangalia na kutathmini kiasi cha fadha zinazohitajika ili ujenzi ukamilike na kufikia tarehe 15/11/2023 kituo hiki kianze kufanya kazi” alisema ndug Katemba.
Mkurugenzi Mtendaji aliongeza kuwa kiasi cha shilingi million 26 kimetengwa kwa ajili ya kumalizia sehemu ndogondogo zilizobaki, fedha ambayo imeletwa kutoka serikali kuu kwa ajili ya afya. Aliwaeleza wanakijiji wa Ilungu jinsi Mhe Rais anavyowapenda na kuwajali kwa kuleta fedha hizo kwa ajili ya maendeleo ya Kata hiyo.
Aidha Mkurugenzi mtendaji amemuagiza mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya Mbeya kuhakikisha gari la wagonjwa linaletwa wiki hii kijijini hapo ili kuweza kuwasaidia wagonjwa na wakinamama wajawazito kuwafikisha hospital kubwa iliopo mbali na Kijiji hicho.
Mkurugenzi mtendaji alimuahidi diwani wa Ilungu kukarabati barabara ambayo diwani huyo ndug Mwakasege Ibrahim alimuomba Mkurugenzi Mtendaji alipotembelea Kata hiyo. “nimemuahidi Diwani kuanzia wiki ijayo barabara ya Kikondo hadi Mswiswi itaanza kufanyiwa ukarabati, sijaahidi lami ila ukarabati uliopo ndani ya uwezo wetu halmashauri tutafanya ili kuweza kukusanya mapato vyema” alisema Katemba.
Ndugu Katemba alitembelea pia kijiji cha Shango na kujionea maendeleo makubwa ya ujenzi wa zahanati ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi, aliwapongeza wanakijiji hao na kuwaomba waendelee na ujenzi huo ila kwa kufata ramani ya ujenzi wa kisasa Zaidi na kuwaahidi kushirikiana nao kuleta maendeleo kijijini hapo.
Mkurugenzi Mtendaji aliwatoa hofu wanakijiji kwa kuwaambia kwamba Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameleta million 42 za maendeleo katika Kata hiyo “Tumshukuru mama etu na Rais wetu wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta million 42 katika kata hii kwa ajili ya Zahanati ya Masese” alisema katemba.
Mwisho Mkurugenzi Mtendaji alifikisha salam za Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuwa anawapenda sana, pia alifikisha salaam za Mkuu wa Wilaya ambaye hii ilikuwa ziara yake ila akapata dharula ya kiserikali.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.