Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imezindua mpango Mkakati wa elimu kwa shule za msingi wenye lengo la kuinua ufaulu kutoka asilimia 61.4 ya mwaka 2017 hadi asilimia 93 kwa mwaka 2018. Akizindua mpango mkakati huo Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya, Ndg, Hassan Mkwawa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kuzigeuza changamoto zinazozikabili Idara ya Eliumu kuwa ni fursa na hatimaye kuja na mpango mkakati huo.
“Kumekuwa na changamoto nyingi ambapo wameamua changamoto hizo kuzigeuza kuwa malengo, na ni chukue fursa hii sasa kuwapongeza kwa sababu tungeendelea kuzichukulia hizi kama ni changamoto tusingekuja na mpango maalumu wa kuja kuinua kiwango cha ufaulu katika shule zetu”
Ndg. Mkwawa amesema kuwa ili malengo ya mkakati huo yaweze kufikiwa ni lazima Halmashauri iusimamie ipasavyo na kuhakikisha kila mdau anatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Ndg. Mkwawa amezindua mpango mkakati huo kwenye kikao cha wadau wa elimu kilichoandaliwa na idara ya elimu msingi. Wadau waliohudhuria katika kikao hicho ni pamoja na wenyeviti wa vijij, watendaji wa vijiji, watedaji kata, waheshimiwa madiwani, walimu wakuu, maafisa elimu kata, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, wazazi, taasisi za fedha, taasisi za kiraia na wazazi.
Awali akiwasilisha mpango mkakati huo ili uweze kujadiliwa, Afisa Elimu Msingi Wilaya, Mwl. Vicent Kayombo amesema kuwa mpango mkakati huo unaitwa Mpango Mkakati wa Elimu wa Isuto wa mwaka 2018. Amesema umepewa jina la Isuto kwa sababu shule ya mwisho kiwilaya inatoka kata ya Isuto, na kuitaja shule hiyo kuwa ni Shule ya Msingi Shitete ambayo haikufaulisha hata mwanafunzi mmoja kati ya wanafunzi 36 waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.
Pia Mwl. Kayombo amesema kuwa mpango mkakati huo umewasilishwa kwa wadau wa Halmashauri nzima ili waweze kuufahamu na kuwa na lengo moja kwani suala la ufaulu wa wanafunzi si suala la kuachiwa walimu pekeyao au idara ya elimu peke yake. Amesema kwa kutambua hilo ndio maana mpango mkakati huo umebeba kauli mbiu inayosema kuwa “Ufaulu wa Juu ni Ushirikiano wa Mimi na Wewe”
Vile vile amesema kuwa mpango mkakati huo umewasilishwa kwa wadau ili weweze kuujadili na kuuelewa kisha kuupeleka kwa wananchi kuutekeleza kwa pamoja, kwani wakiulewa wao kama viongozi itakuwa ni rahisi kutekelezwa.
“Leo sasa mpango huu, umeletwa mbele ya wadau wa elimu, wadau wa elimu ambao ni viongozi ili nao waweze kuupitia, kuachambua, ili maazimio yake, yatakuwa sasa ndio dira ya kushuka kule chini kwa wananchi. Idara ya Elimu Msingi inaamini kwamba wananchi wako tayari, wazazi wako tayari, tatizo ni sisi viongozi. Viongozi tukiwa na uelewa wa pamoja tukashusha maelekezo, tukawa mfano kule chini, tunaamini wazazi watatuunga mkoni kikamilifu, na hatimaye tutafikia malengo ambayo tumejiwekea.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Ntokani akifunga mjadala baada ya wadau kuujadili na kuukubali mpango mkakati huo amesema kuwa kilichobaki sasa ni kufanya kwa vitendo. Na kuwaomba wadau kudumisha mshikamano na ushirikiano katika kutatua changamoto za elimu na kuzigeuza kuwa fursa kama mpango mkakati ulivyoelezea ili lengo liweze kufikiwa.
“naomba sana tujitahidi, baada ya kutoka hapa twende tukafanye kazi ya kushikana na kushikamana kwa kuhakikisha tunaziondoa hizo changamoto zilizopo kwenye maeneo yetu”
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.