Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi 197,306,620/= baada ya kushinda kesi 5 katika mahakama mbalimbali nchini. Hayo yamebainishwa na mwanasheria wa halmashauri, Wilson Nyamunda wakati akisoma taarifa ya kitengo cha sheria katika mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika mei 4, 2018 kwenye ukumbi wa halmashauri.
Akizitaja kesi hizo Nyamunda amesema kesi ya kwanza ni ya madai ya makusanyo ya ushuru wa mazao kati ya halmashauri ya Wilaya ya Mbeya dhidi ya Thob Traders Ltd. Kesi Na. 9/2013 iliyokuwa mahakama kuu kanda ya Mbeya ambapo halmashauri imeshinda na kufanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi 118,000,000/=
Amesema kesi ya pili ni kesi Na. 103/2017 iliyokuwa baraza la ardhi na nyumba wilaya, kati ya Erick Mahenge na wenzake 66 wakiishitaki halmashauri kuwapandishia kodi ya pango katika vibanda vya biashara Mbalizi, kesi hii imefutwa na Halmashauri imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi 40,200,000/= zinazotokana na kodi hiyo.
Kesi ya tatu ameitaja kuwa ilikuwa tume ya usuluhishi wa migogoro kati ya Meshaki Kapange dhidi ya halmashauri ikiwa ni madai ya kusitishiwa mshahara kiasi cha shlingi 6,571,520/= kesi hii imetolewa uamuzi kwa tume kulitupilia mbali pingamizi la mlalamikaji.
Nyamunda ameitaja kesi ya nne kuwa ni kesi kati ya halmashauri dhidi ya Esthlajen Co. Ltd kesi ya madai Na. 36/2016 ikiwa ni madai ya makusanyo ushuru wa magulio kwa mwaka 2014/2015. Kiasi kinachodaiwa ni shilingi 13,035,100/= Nyamunda amesema kesi hii imeisha ambapo halmashauri imeshinda na sasa imeomba nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi kwa ajili ya kukaza hukumu.
Pia ameitaja kesi ya tano kuwa ni kesi ya madai Na. 45 kati ya Halmashauri dhidi ya Obadia Haruna ikiwa ni madai ya ushuru wa stendi Mbalizi kiasi cha shllingi 19,500,000/=
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya, Mhe. Mwalingo Kisemba amewapongeza wataalamu wa halmashauri hususani kitengo cha sheria kwa kuiongoza halmashauri kushinda kesi hizo na kuisadia kuokoa kiasi hicho cha fedha.
Aidha Mhe. Kisemba amesema kuwa kesi nyingi zilizokuwa zinaikabili halmashauri zimetokana na madai ya ushuru ikiwa imesababishwa na mawakala kutowasilisha ushuru huo kwa wakati. Hivyo amesema kwa sasa halmashauri imejipanga kutozalisha kesi hizo kwa sababu sasa halmashauri inakusanya yenyewe ushuru huo bila ya kutumia mawakala kama ilivyokuwa awali.
“lakini pia huko nyuma tulikuwa tunafanya kazi na mawakala sasa hivi tunakusanya mapato wenyewe na tumeona mafanikio ya kutosha. Halmashauri yetu inamaeneo mengi ya kuzallisha nadhani tukijikita kuhakikisha kila ushuru unaopaswa kutolewa utakuwa unatolewa hatutafika tena mahakamani”
Naye diwani wa viti maalumu, Mhe. Aida Haule amesema kuwa halmashauri kwa kushinda kesi hizo imesaidia kuokoa pesa ambazo zitatumika kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo iliyosimama kutokana na ukosefu wa fedha ikiwemo miradi ya elimu, afya na maji.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.