Ujenzi wa bandari kavu Inyala, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya umetajwa kuwa ni nguzo muhimu ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi zinazopakana nazo upande wa nyanda za juu kusini ikiwemo Malawi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla kwenye ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alipotembelea bandari ya Itugi katika ziwa Nyasa kukagua ujenzi wa meli ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mzigo wa tani 200. Na kukagua meli mbili katika bandari ya Kiwira (MV Njombe na MV Ruvuma) zenye uwezo wa kubeba mzigo wa tani 1,000 kila moja.
Makalla amesema, kukamilika kwa meli hizo kumeongeza kasi ya kusafirisha mizigo toka Tanzania kwenda Malawi, lakini ujenzi wa bandari kavu Inyala ndio unategemewa kufanya mageuzi ya usafirishaji mizigo nchini kwa kupitia njia ya reli ya TAZARA ambayo gharama yake ni nafuu zaidi kuliko njia ya barabara kama inavyotumika hivi sasa.
"Mhe. Makamu wa Rais, ujenzi wa bandari kavu Inyala ni nguzo muhimu katika ukuaji wa kiuchumi wa mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla, kwani itasaidia kusogeza Huduma za bandari toka Dar es salaam hadi Mbeya hali itakayowapunzia gharama za usafiri wateja wetu wa nchi za Malawi, Zambia na Kongo"
Aidha Makalla, amemuomba Makamu wa Rais kuihimiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuongeza kasi katika ujenzi wa bandari hiyo kwani uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya umetenga eneo la hekari 110 ambapo TPA imeliridhia, na hatua za awali ya kulitwaa eneo zimekamilika, kinachosubiriwa sasa ni TPA kulipa fidia na kuanza ujenzi.
Kwa upande wake Makamu wa Rais, ameupongeza uongozi wa mkoa pamoja na halmashauri kwa kuanzisha mpango wa ujenzi wa bandari kavu Inyala kwani itaongeza mapato ya halmashauri na mkoa.
Pia Mhe. Samia amewataka wananchi wa mkoa wa Mbeya kufanya kazi kwa bidii na ubunifu wa kuzalisha mazao kwa viwango vya kimataifa ili kuweza kutumia bandari kavu tarajiwa ya Inyala pamoja na meli za mizigo zilizopo bandari ya Kiwira kusafirisha mazao yao nje ya nchi.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.