Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2018, Ndg. Charles Kabeho amekabidhi mkopo wa shilingi milioni 105 kwa vikundi 18 vya wanawake vilivyopata shilingi milioni 49 na vikundi vya vijana 9 vilivyopata shilingi milioni 56. Kabeho amekabidhi mkopo huo wakati Mwenge wa Uhuru ulipoenda kukagua shughuli za kikundi cha vijana wafugaji wa kuku “COFAPS”
Akikabidhi mkopo huo Kabeho, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kutekeleza kwa vitendo sera ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ya mwaka 2004 inayoelekeza halmashauri zote nchini kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana.
“Niipongeze Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kuweza kutenga asilimia kumi ya mapato yake kwa ajili ya kuweza kuvikopesha vikundi”
Aidha kabla ya kukabidhi mikopo hiyo, Kabeho alifanya zoezi la kuvihakiki vikundi vyote 27 vilivyopangwa kupatiwa mikopo. Katika ukaguzi huo vikundi 16, vikiwemo vya wanawake 13 na vijana 3 vilikaguliwa na kukabidhiwa hati za mikopo. Vikundi 11 vikiwemo vya wanawake 5 na vijana 6 havikuweza kukaguliwa kwa sababu mbalimmbali zikiwemo kutofika kwa wakati katika eneo la tukio. Na sababu nyingine ni wanavikundi kufika wachache badala ya kufika wote kama alivyoagiza kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2018.
kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2018, Ndg. Charles kabeho akikagua kitambulisho kimojawapo cha wanakikundi cha vijana kabla hajatoa mkopo kwa vijana hao
Kwa vikundi ambavyo hakuvikaguliwa, Kabaho amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, kuvihakiki kama vinasifa ya kupatiwa mkopo, na akikuta kikundi ambacho hakina sifa, fedha zote zirudishwe halmashauri kwa ajili ya kukopesha vikundi vingine vyenye sifa.
Akipokea agizo hilo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Paul Ntinika amesema kwamba atavikagua vikundi hivyo ndani ya siku 5 kwa kushirikiana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya. baada ya kuvikagua atawasilisha taarifa kwa maandishi kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2018 ili aweze kuzifikisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dakt. John Pombe Magufuli.
Awali akisoma taarifa ya mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Afisa Maendeleo Wilaya, Zena Kapama amesema kwamba halmashauri imejiwekea mkakati wa kutoa mikopo hiyo kila robo, tofauti na hapo awali ambapo ilikua inatoa kwa mkupuo.
Amesema mkopo uliokabidhiwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa vikundi 16 ni wa robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Amesema mpaka sasa halmashauri imetoa jumla ya shilingi milioni 435 kwa vikundi 135 vya wanawake na vijana.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.