Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Paul Ntinika amefungia mgodi wa kuchimba madini aina ya mabowo uliopo kijijii cha Igalukwa kata ya Itawa. Mkuu wa Wilaya amefungia mgodi huo kwa kosa la kutofuata sheria na kanuni za uchimbaji wa madini nchini zinazomtaka mchimbaji kuwa na vibali kutoka Wizara ya Nishati na Madini, barua ya utambulisho kutoka ofisi ya madini kanda ikimtambulisha kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya na Kijiji.
Mh. Ntinika amefungia mgodi huo alipofanya ziara ya kushtukiza akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Igalukwa kuwa kuna watu wenye asili ya asia (wachina) wamevamia mashamba yao na kufanya shughuli za uchimbaji bila ya kuwa na taarifa yoyote.
“Tumepokea malalamiko toka kwa wananchi wa kijiji cha Igalukwa kata ya Itawa pamoja na Mheshimiwa diwani kuwa maeneo yao yamevamiwa na watu wasiokua na taarifa nao ambao wanachimba madini. Bahati nzuri tumefika hapa na tunaona mitambo mikubwa kweli na baadhi ya maeneo kuchimbwa na kuchongwa barabara. Na hata ukiangalia kwa macho tunashuhudia kuwa eneo hili limezungukwa na mashamba ya wananchi, sasa tumekuja ili kuona hawa watu wameingiaje katika eneo hili…”
Baada ya kuzungumza na wananchi Mh. Ntinika alizunguka kukagua mgodi huo na kugundua kuwa mgodi upo karibu na chanzo cha maji lakini waendeshaji wa mgodi huo hawajachukua hatua yoyote ya kukilinda chanzo hicho na badala yake wanatupia mabaki ya mawe na mchanga kwenye chanzo hicho hali inayohatarisha uhai wake. Baada ya kugundua uharibifu huo Mh. Ntinika aliwauliza watumishi wa mgodi huo na kukiri kuwa huo ni uharibifu unaofanywa na kampuni yao.
Kisha Mh. Ntinika alihitaji kuwaona wamiliki wa mradi huo lakini kwa bahati mbaya hawakuwepo mgodini hapo na wasimamizi waliokuwepo (wachina) hawakujua kuzungumza lugha ya Kiswahili wala Kiingereza, ndipo alipopewa namba ya mtu aliyefahamika kwa jina la Peter ambaye anafanya kazi katika mgodi huo kama msemaji wa kampuni. Baada ya kuwasiliana naye kwa simu Mh. Ntinika akatoa agizo la kufungia mgodi huo mpaka taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Pia akifungia mgodi huo Mh. Ntinika ameagiza mawe ambayo yamechimbwa yasisafirishwe, wananchi kupitia Halmashauri ya Kijiji cha Igalukwa watasimamia ulinzi wa mgodi huo.
“Kama nilivyokuwa nawasiliana na msemaji wa kampuni ambaye anaongea lugha ya Kiswahili, kwa vile wenzetu hawajui lugha ya Kiingereza wala Kiswahili sasa uwaambie kwamba shughuli zote zinasimama mpaka watakapowasilisha taarifa yao kwa nini wamekiuka taratibu na hawajashirikisha kijiji, baada ya kupokea ndio tutatoa tamko lingine la shughuli kuendelea. Shughuli zote kuanzia leo zimesimama…. Wananchi wa eneo hili wataendelea kulinda, hakuna fujo itakayotokea hawa wakae kwa amani, wananchi nao wakae kwa amani. Mawe yasichukuliwe mpaka watakapo wasilisha taarifa”
Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Itawa, Elia Mwampamba amemshukuru Mh. Ntinika kwa uamuzi aliochukua kwa kusema uamuzi huo unalenga kuleta ufumbuzi na suluhisho kwa wananchi ambao mashamba yao yameharibiwa
.“Ukweli uliopo ni kwamba kuna baadhi ya mashamba ya wananchi yameharibiwa hovyo bila kupewa fidia yoyote nipenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mku wa Wilaya baada ya kutoa agizo kwamba shughuli yoyote isiendelee hadi atakapokutana na uongozi wa kampuni hii kuangalia walikuje kujeje na kwa nini wameharibu mashamba ya watu na wananchi wanapata vipi fidia zao kwa wakati. Hivyo nishukuru sana kwa Mkuu wa Wilaya, naamaini wananchi haki yao wanaenda kuipata”
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.