Watumishi watatu kati ya wanne waliofukuzwa kazi Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wamerejeshwa kazini. Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amosi Makalla wakati akiongea na Waheshimiwa Madiwani kwenye mkutano wa wa dharula wa Halmashauri hiyo. Mhe. Makalla amewataja watumishi hao watatu walirejeshwa kazini kuwa ni; Edwin Magiri ambaye alikuwa Kaimu Mhandisi Ujenzi, Eliada Misana aliyekuwa Kaimu Afisa Ugavi na Manunuzi pamoja na Betty Mlaki aliyekuwa Afisa Elimu Msingi.
Akitoa taariifa hiyo Mhe. Makalla amesema kuwa watumishi hao wamerudishwa tena kwenye utumishi wa umma baada ya kushinda rufaa katika Tume ya Utumishi wa Umma waliyokata kupinga kufukuzwa kazi. Amesema Tume kulingana na Mamlaka iliyonayo kisheria chini ya kifungu cha 25 cha Sheria za Utumishi wa Umma sura ya 298 pamoja na sura ya 60 ya kanuni za Utumishi wa Umma, Tume imewarudisha kazini watumishi hao baada ya kupitia rufaa zao na kubaini kuwa taratibu hazikufuatwa wakati wanafukuzwa kazi na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya WIlaya ya Mbeya.
“Nimeletewa kopi ya barua watumishi wote wamerejeshwa tena, na kwamba maamuzi yenu hayakuzingatia taratibu. Ninazo kopi zote za barua hapa na wameeleza mazingira yote ambao watumishi hawa wamekosewa kufukuzwa kazi”
Pia Mhe. Makalla amewaasa Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuzingatia ushauri unaotelewa na wataalamu pamoja na ule unaotoka ngazi za juu. kwani laiti wangelifuata ushauri waliopewa awali na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, pamoja na Ushauri wa Waziri Mkuu alioutoa wakati anaongea na watumishi wa Umma wa Wilaya ya Mbeya tarehe 31 Julai, 2017 Hayo yote yasingetokea. Na kukitaja kitendo cha wafanyakazi waliofukuzwa kazi na Baraza la madiwani kurejeshwa kazini kuwa ni aibu kwa Waheshimiwa Madiwani.
“Sasa najiuliza kama tuliwashauri kuanzia mwanzo haya yasingetokea, Kama mngefuata ushauri wa kwanza tulioutoa haya yasingetokea, mkakataa ushauri wa Mkoa, mkakataa ushauri wa Waziri, mkakataa maelekezo ya Waziri Mkuu. Tarehe 28 Agosti, 2017 nilikuja kuwatahadharisha sasa leo yametokea, aibu kwenu”
Mhe. Makalla amesema Serikali haiko tayari kumtetea mbadhilfu yeyote na wala haifurahishwi na vitendo vya ufujaji wa pesa za Umma, lakini hatua zinapochukuliwa dhidi ya wabadhilifu hao ni lazima Sheria, Kanuni na Taratibu zizingatiwe ili kusiwe na mtu yeyote atakayeonewa.
“nataka kuwahakikishia serikali hii yote na sisi tuliopewa dhamana hii hatuwezi kukubali ubadhilifu, hatuwezi kukubali ufisadi, hatuwezi kukubali fedha za umma zikachezewa , lakini tunapochukua hatua tusiwaonee watu hii mnajenga taswira mbaya kwa serikali kwamba mnataka kuonesha kwamba watu wanao uwezo wa kuonewa”
Akiongea wakati wa kufunga Mkutano huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Mhe. Mwalingo Kisemba amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwapa taarifa juu wa watumishi waliorejeshwa kazini na kusema wala wao ahawana kinyongo chochote kwa sababu kukata na kushinda rufaa ni haki ya Mkutumishi na hayo yote yamefanyika kwa mujibu wa Sheria.
Pia ameongeza kwa kusema kwamba wakati madiwani wanachukua hatua za kuwafukuza kazi watumishi hao walifanya baada ya tuhuma kuthibitika kupitia kamati mbalimbali zilizoundwa na Waheshimiwa Madiwani pamoja na kamati iliyoundwa na Serikali.
“nichukue nafasi hii kumshukuru Mkuu wa Mkoa kuja kutuletea ujumbe wa watumishi tuliokuwa tumewafukuza kisha wakakata rufaa wameshinda na kwa sababu ilikua ni ujumbe niseme tumepokea kwa mikino miwili na sisi kama madiwani kama baraza kazi yetu ya msingi tuliifanya na haki ya mtuishi ni kukata rufaa wamekata rufaa wameshinda wala hatuna tatizo lolote kwa sababu ndio utaratibu wa sheria”
“Tumeletewa tumefanya kwa mujibu wa Serikali ziliundwa kamati mbalimbali na tuhuma zilithibitika na tuliamua kwa sababu tuliridhika kwamba tuhuma zimethibitika kutoka kwenye kamati ambazo zilikua zimeundwa na nyigine ya mwisho wala hakuna hata diwani mmoja aliyeingia lakini tuhuma zilithibitika. Sasa kushinda rufaa ni haki ya mtu na sisi wala hatuna tatizo”
Watumishi waliorejeshwa kazini walifukuzwa kazi na Baraza la madiwani lililofanyika mwezi Septemba mwaka 2016 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Usongwe.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.