Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya yaahidi kujenga bweni kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Abihudi Fungamtama amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya itawasilisha mpango wa kujenga bweni kwa ajili ya wanafunzi wenyemahitaji maalum ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili. Hayo ameyasema wakati wa ufunguzi wa kituo cha wanafunzi wenyemahitaji maalum katika Shule ya Msingi Nsongwe Juu iliyopo kata ya Ijombe. Ndg. Fungamtama amesema kuwa watoto wenyeulemavu wanakabiliana na changamoto nyingi ikiwemo kubaguliwa na jamii na wengine kufichwa majumbani hali inayosababisha watoto hao kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu.
“kuna baadhi ya wazazi na walezi wanaona ni mkosi katika familia kupata mtoto mwenye ulemavu na hivyo kujichukulia uamuzi wa kumfungia mtoto huyo ndani kwa lengo la kuepuka aibu. ’Niwaombe wazazi,walezi ,pia viongozi wa mitaa na vitongoji kusaidiana na serikali kuwafichua watoto hawa wanaofichwa, na sisi kama serikali tutahakikisha tunaweka mazingira mazuri ya watoto hao kupata elimu bora”
Jambo la kwanza tunalolofikiria ni kuwasilisha mpango wa kujenga mabweni walau kwenye shule moja yenye kituo kama hiki katika vikao vya Waheshimiwa madiwani, na tunaimani watatuunga mkono. Kwa Halmashauri yetu ya Mbeya, ukijumlisha na hiki kituo tunachokifungua leo tunakua na vituo vitatu vya kutolea elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, lakini hakuna kituo hata kimoja chenye bweni hali inayosababisha wazazi na walezi kushindwa kuwapeleka watoto wao shule kwa madai ya umbali. Hivyo tukisha jenga bweni itakua ni rahisi kwa mzazi ama mlezi kumuanzisha shule mtoto wake kwa sababu hatopata tena usumbufu wa mara kwa mara wa kumpeleka na kumfuata mtoto wake shule, na wala hakutakua tena na kisingizio cha umbali” Amesema Fungamtama
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Ndg. Abihudi Fungamtama akikata utepe kwenye mlango wa darasa la walemavu shule ya msingi Nsongwi Juu kuashiria kuzindua kituo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Awali akisoma taarifa ya kituo hicho, Afisa Elimu, Elimu Maalum ya Ulemavu ,Wende Mbilinyi amesema kuwa kituo hicho kina jumla ya wananfunzi 21 wenye ulemavu wa aina mbalimbali ikiwa uoni hafifu, vipofu, viziwi, ulemavu wa ngozi, ulemavu wa viungo pamoja na ulemavu wa akili. Amesema kituo hicho kimeanzishwa kikiwa na walimu watatu waliobobea katika taaluma ya kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Naye Kaimu Afisa Elimu Wilaya, Ndg. Aliamini Juma ametoa pongezi zake kwa kamati ya Shule pamoja na wazazi kwa kuanzisha mchakato wa kuanzishwa kituo hicho jambo linalotoa fursa kwa wanafunzi wenye ulemavu kapata elimu. Pia amesema uwepo wa kituo hicho katika shule hiyo kitakua ni chachu kwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwapeleka watoto wao shuleni hapo kwa ajili ya kupata elimu.
Bi. Mbole Mbiga mlezi wa Mtoto mwenye ulemavu wa macho amesema amefurahishwa kwa kuanzishwa kituo hicho kwani sasa itakua ni rahisi kwake kumpeleka mwanae shuleni hapo. Amesema mjukuu wake mwenye umri wa miaka 15 tangu azaliwe hakuwahi kupata elimu, lakini aliposikia kuwa kwenye Shule ya Msingi Nsongwi juu kumeanzishwa kituo cha kutolea elimu kwa wanafunzi wenye ulemavu imemlazimu kufika kwa ajili ya kumuanzisha shule. “Mwanzo nilikua sijui kama mtoto mlemavu kama huyu anaweza akasoma, hivyo nilikaa naye nyumbani kwa muda wote bila ya kumpeleka shule, lakini niliposikia kwamba katika shule hii iliyopo kijijini kwetu kumeanzishwa kituo cha kuwafundisha walemavu nami nimeona sina budi kumleta mjukuu wangu ili aanze masomo, na ndio maana nimefika hapa kwa ajili ya kumuandikisha shule. Amesema
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.