Waheshimiwa Madiwani wakumbushwa kutekeleza ahadi zao
Takribani miezi 19 sasa imepita sawa na mwaka mmoja na miezi saba tangu uchaguzi mkuu ufanyike tarehe 25 Oktoba 2017. Uchaguzi Mkuu nchini hufanyika kila baada ya miaka mitano ambapo raia wa Tanzania wenye umri kuanzia miaka 18 hupata fursa ya kuwachagua wawakilishi wao; yaani waheshimiwa madiwani, wabunge pamoja na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Katika uchaguzi wa 25Oktoba 2017 wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya nao walipata fursa hiyo ya kuwachagua wawakilishi wao ambapo kwa ngazi ya kata waliweza kuwachagua waheshimiwa madiwani 38, kati ya hao 28 waliogombea kwenye kata na 10 walipita kwa nafasi ya Udiwani Viti Maaluma.
Bila chembe ya shaka yoyote wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya waliwachagua viongozi hao baada ya kuridhishwa na ahadi walizozitoa wakati wa kampeni iliyofanyika kwa miezi mitatu kabla ya tarehe ya uchaguzi. Bw. Costantino Mushi Afisa Serikali za Mitaa toka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya amewakumbusha Waheshimiwa madiwani kutekeleza ahadi zao walizoziahidi wakati wa kampeni ili kuwajengea imani wananchi na serikali waliyoichagua.
Bw. Mushi ameyasema hayo kwenye Mkutano wa baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya alipomwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bi. Rehema Mtunguja. Bw. Mushi amesema ahadi nyingi walizozitoa madiwani zinalenga kuwapelekea maendeleo wananchi katika maeneo yao, hivyo wakati muafaka wa kutekeleza ahadi hizo ni sasa kabla ya kusubiri uchaguzi mwingine utakaofanyika mwaka 2020.
Bw. Mushi amesema ili kutekeleza ahadi hizo kwa urahisi ni vyema waheshimiwa madiwani wakaweka maslahi ya wananchi mbele badala ya kuangalia maslahi yao binafsi. Pia amesema ni vyema madiwani wakaongeza nguvu katika kukusanya mapato ili fedha zitakazo patikana zipelekwe kutekeleza ahadi hizo.
“Tuweke maslahi ya wananchi mbele badala ya maslahi yetu sisi binafsi, tufanye kazi kwa kumuangalia mwananchi wa kawaida ambaye ametuleta katika baraza hili. Na niseme kwamba kunaahadi nyingi mmeahidi kule kwa wananchi, siku zinayoyoma, mapato pengine hayakidhi, miradi haitekelezeki sasa mtapoteza muda na watu ambao hawaisaidii tena hii Halmashauri badala ya kukazana kukusanya mapato zaidi na kuelekeza kule kwa wananchi ili zile ahadi ulizoahidi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Taifa wa mwaka 2015 ziweze kutekelezeka”
Pia Bw. Mushi amesema ili Halmashauri hii iweze kufikia lengo katika kukusanya mapato ni vyema waheshimiwa madiwani wakashirikiana wataalamu.
“Napenda kusisitiza katika kukusanya mapato, wiki iliyopita nimeona mmefikia zaidi ya asilimia 60 la lengo lenu la mwaka. Lakini muda umekwisha na tumeagizwa kufikia asilimia 100 ikifika tarehe 30 Juni. Kama hamkufikia asilimia 100 ni lazima muweke sababu za msingi kwanini hamkufikia lengo. Kwa hiyo kwa hili ninaomba mshirikiane na watendaji wala msiwaachie wao wenyewe”
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.