Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwasaka na kuwakamata watu wote waliohusika kuwapa mimba wanafunzi.
Makalla, ametoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Inyala kata ya Inyala wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo iliyofanywa kwa nguvu za wananchi katika kata hiyo.
Aidha Mkuu wa mkoa amesema kuwa, haivumiliki kuona mwanafunzi amesitishiwa masomo kwa kupewa ujauzito kwani serikali inatumia gharama kubwa kuwasomesha kupitia mpango wa elimu bila malipo. Hivyo amewataka wazazi na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kuhakikisha wale wote waliohusika kuwapa ujauzito wanafunzi wanatiwa mbaroni.
“ Kwa hiyo suala hili la kuwapa watoto mimba, niwaombe wazazi na jamii kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la kuwabaini wahusika”
Akipokea agizo hilo kwa niaba ya kamati ya ulinzi na usala Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Paul Ntinika amewataka wale wote aliohusika kujisalimisha wenyewe mikononi mwa polisi kabla kamati ya ulinzi na usalama haijawabaini.
Awali alipotembelea shule ya sekondari Imezu kukabidhi viti 150 vyenye thamani ya shilingi 6,762,000/= vilivyotengenezwa na wazazi wa shule hiyo. Mkuu wa shule, Mwl. Tibus Makona amesema kuwa licha ya mafanikio waliyoyapata bado shule inakabiliwa na changamoto ya mimba ambapo kwa mwaka huu hadi kufikia Mei 30 jumla ya wanafunzi watano (5) wamepata ujauzito, kati yao watatu ni wa kidato cha nne na wawili ni wa kidato cha pili na kwanza.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.