Halmashuri ya wilaya ya Mbeya imewarejesha kazini watumishi 72 walioondolewa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara kwa kukosa sifa ya cheti cha kufaulu mtihani wa elimu ya kidato cha nne.
Akizungumza na watumishi hao katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya, Mkurugenzi Mtendaji, Amerchioly Kulwizila amesema watumishi hao wamerejeshwa kazini ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na utawala bora), George Mkuchika alilolitoa bungeni tarehe 9 Aprili, 2018 katika kikao cha kuwasilisha bajeti ya wizara hiyo.
Aidha, Kulwizila amewahakikishia watumishi wote waliorejeshwa kazini kupatiwa stahiki zao kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni. Pia amewataka kufanya kazi kwa uzalendo katika kuwatumikia wananchi.
Akisoma waraka wa kuwarudisha kazini watumishi hao Afisa Utumishi, Bi. Sikijua Kihwelo amesema watumishi waliorudishwa katika utumishi wa umma ni wale ambao walioajiriwa kwa cheti cha darasa la saba kabla ya mei 20, 2004. Amesema zoezi hili haliwahusu watumishi walioondolewa kazini kwa kosa la kughushi cheti cha elimu ya kidato cha nne na waliotoa taarifa za uongo katika fomu za kupima utendaji kazi kwa watumishi wa umma.
Watumishi hao waliondolewa kazini mwezi Septemba, 2017 kutokana na agizo la Serikali la kuwatoa katika mfumo wa malipo ya mishahara watumishi walioajiriwa kabla ya mei 20, 2004 kwa kukosa sifa ya ufaulu wa kidato cha nne kama waraka na. 1 wa mwaka 2004 ulivyokuwa unataka.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.