Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa amesema katika mwaka huu wa fedha (2017/2018) Serikali itaendelea kupeleka fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya. Miongoni mwa miradi iliyotajwa na Waziri Mkuu ambayo itapelekewa fedha ni pamoja na miradi ya kada za Afya, Maji na nishati ya Umeme. Mh. Waziri Mkuu, amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya kauli mbiu ya “HAPA KAZI TU” inadhamira ya dhati kuwahudumia wananchi kwa kuboresha hudama zitolewazo serikalini.
Kwenye huduma ya kusambaza maji Mh. Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata maji safi na salama. Amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa Mamlaka za Maji nchini pamoja na Idara za Maji katika Halmashauri ambapo kwa nchi nzima zimetengwa Shilingi Bilioni 237.800. fedha hizo zitatumika kutafuta vyanzo vipya vya maji kwa sehemu ambazo bado hazina miradi ya maji na pia kuiongezea uwezo miradi ya maji ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa ya ongezeko la watu. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inatarajiwa kupewa kiasi cha fedha Shilingi Milioni 622.
Kwenye huduma za afya Mh. Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya nchini kwa kutenga fedha za kununulia dawa ili kuhakikisha mwananchi anapofika katika kituo cha kutolea huduma za afya hakosi dawa. Pia Waziri Mkuu amefahamisha kwamba Mkoa wa Mbeya utapata Bilioni 4.225, ambapo katika fedha hizo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya itapata Milioni 836.1
“Tunahitaji kila mahali pawe na dawa hapa kwenu tutawatengea bilioni 4.225 kimkoa… Halmashauri ya wilaya ya Mbeya najua wadau mko hapa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya tumewatengea milioni 836.1 kwa hiyo tunatarajia fedha hizo za dawa ambazo huwa zinatoka hazina ubishi zifike Mbeya vijijini, zifike hapa jiji na wanunue dawa kwenye zahanati zote, vituo vya afya na hospitali ya wilaya. Kwa hiyo ndugu watanzania kwenye sekta ya afya tunaenda vizuri, tumejipanga vizuri na tunaendelea kuhakikisha kwamba watanzania wanakua na afya njema”
Kuhusu nishati ya umeme Mh.Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha kuwa vijiji vyote vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya vinaunganishwa na nishati ya umeme. Halmashauri ya Mbeya inajumla ya vijijii 152, kati ya vijiji hivyo vijiji 122 tayari vimeunganishwa na nishati ya umeme kupitia mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA). Waziri Mkuu amesema vijiji 30 vilivyobaki navyo vitaunganishwa na nishati ya umeme kwani bajeti yake ishatengwa na Serikali imepeleka mkandarasi kwa ajili ya kufanya usanifu.
Pia Mh. Waziri Mkuu amesema gharama za mtu kuomba kuunganishwa na nishati ya umeme zimepungua kutoa Tsh 380,000/- hadi kufikia TSh 27,000/- Amesema hii imeamriwa na Mh. Raisi wa Jamhuri ya Muungano, Dk John Pombe Magufuli yeye mwenyewe ili kumhakikishia kila mtanzania anapata fursa ya kuunganishwa na huduma hii muhimu.
“Mbeya vijijini bado vijiji thelathini (30) tu, tunamkandarasi tumemleta tunataka kuweka umeme kila kijiji, hivi vijiji thelathini (30) vya Mbeya vijijini vyote tunafunika umeme, na Raisi katika hili amesema watanzania hawa mpaka yule wa chini lazima apate umeme, atapataje kama malipo ni Tsh 380,000/- amesema hakuna kulipa 380,000/- sasa ni Tsh 27,000/”
Pia Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga na itatekeleza kuhakikisha nchi nzima inaunganaishwa na nishati ya umeme, hata katika maeneo ambayo vijiji vyake vipo mbali na vina jiografia ngumu ya kuunganishwa na nguzo za umeme, Serikali itapeleka mafundi kufunga umeme wa nishati ya jua.
“… Na tukigundua kwamba kuna kijiji kipo kule, ni mbalii kutundika nguzo mpaka kule ni gharama kubwa, tunakwenda tunabandika sola kila nyumba huko huko juu” Amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hizo alipokua akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbeya katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Luanda Nzovwe CCM jijini Mbeya. Waziri Mkuu amefanya ziara ya siku nne mkoa wa Mbeya iliyoanza tarehe 29/07/2017 na kumalizika tarehe 01/08/2017. Katika ziara hiyo Waziri Mkuu ametembelea Wilaya ambazo ni; Kyela, Rungwe, Mbeya pamoja na Chunya.
Mbaliz Road
Sanduku la posta: 599
Simu ya mezani: 025-2502260
Simu ya mkononi: 0762210758
Baruapepe: ded@mbeyadc.go.tz/info@mbeyadc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya District Coucil . All rights reserved.